Kutokana na habari zilizotufikia hivi punde ni kwamba msanii  wa filamu nchini Tanzania, Elizabeth Michael aka Lulu ambaye yuko mahabusu katika gereza la Segerea jijini Dar es Salaam, hatotoka leo kama ilivyoandikwa na vyombo mbalimbali vya habari. Hii ni kutokana na kutotimiza masharti yote ya dhamana ikiwa ni pamoja na hati za kusafiria pamoja na dhamana ya milioni 20.

Wiki iliyopita mawakili wa muigizaji huyo waliwasilisha maombi ya dhamana kwa mahakama hiyo kuu ya Tanzania.

Wanasheria hao Peter Kibatala, Kennedy Fungamtama na Fulgence Massawe waliomba dhamana hiyo itolewe haraka kwakuwa muombaji amekaa mahabusu kwa zaidi ya miezi saba na kwamba kosa lake linaweza kupewa dhamana.

Lulu anakabiliwa na kesi ya kumuua bila kukusudia Steven Kanumba April 7, 2012, huko Sinza Vatican, jijini Dar es Salaam.

Kanumba alidaiwa kuwa kwenye ugomvi na Lulu aliyekuwa mpenzi wake nyumbani kwake Sinza.